HOTUBA YA NAIBU KATIBU MKUU CHADEMA Ndg. ZITTO KABWE KWA WANACHADEMA WANAOISHI MAREKANI – MARYLAND, VIRGINIA NA DC
27.05.2012
Tumekutana
leo wakati ambao Taifa letu lipo katika mpito wa mambo mengi sana.
Kufuatia shinikizo kubwa kutoka chama chetu cha CHADEMA na asasi
nyingine za kiraia ikiwemo viongozi wa dini, tupo katika mchakato wa
kuandika upya katiba ya nchi yetu. Lakini pia kuna muamko mkubwa sana wa
haki za kiraia na haki za kisiasa katika Taifa letu hivi sasa.
Watanzania, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu,
wameamka na kutaka mabadiliko ya kisiasa na hasa kutaka kabisa uongozi
mpya wa nchi kutoka chama kingine tofauti na chama kinachoongoza hivi
sasa. Huu mpito pia, Mpito wa kutoka chama kimoja hodhi kwenda mfumo wa
kweli wa vyama vingi vya siasa. Watanzania wameamka sana kujua
rasilimali za nchi yao na kutaka kutokomeza rushwa na ufisadi na
matumizi mabaya ya utajiri wa nchi. Huu ni mpito wa kutoka viongozi
wanaojali maslahi yao binafsi na kwenda kwa viongozi wawajibikaji na
wenye uchungu wa kuendeleza nchi yetu na watu wake.
Mpito
wowote unapaswa kuongozwa vyema. Unapaswa kushirikisha wananchi wote
bila kujali wapo sehemu gani ya Dunia. Chama chetu kipo mstari wa mbele
kuongoza mpito tulionao Tanzania. Licha ya kuongoza juhudi za kuwa na
Katiba mpya itakayohakikisha HAKI na Wajibu wa Watanzania, lakini pia
tumekuwa tukiendelea kupambana na rushwa na ufisadi. Pia tumekuwa
tukiendelea kuhakikisha utajiri wa nchi yetu unatumika kwa manufaa ya
Watanzania. Hatujatetereka hata kidogo na hatutateterekea kuhakikisha
Watanzania wanakuwa na Taifa lenye demokrasia iliyokomaa, lenye
maendeleo na ustawi wa watu wake (Developmental Democratic State).
Licha
ya kwamba tupo Upinzani, lakini hatua mbalimbali tulizochukua zimeleta
mabadiliko makubwa katika nchi yetu. Kuanzia vuguvugu la Buzwagi mpaka
kuibuliwa kwa maskandali ya EPA na mpaka kutajwa kwa orodha ya Mafisadi
nchini pale MwembeYanga. Hata hivi karibuni juhudi za Bunge kutaka
Uwajibikaji Serikalini zilizoongozwa na CHADEMA zimeleta mabadiliko.
Inawezekana mabadiliko hayo sio kama tutakavyo, sio kamili, lakini ni
hatua ambayo tumepiga. Tutaendelea kama chama cha siasa sio tu kusema na
kupiga kelele kuhusu uoza uanaofanyika Serikalini (maana ndio kazi yetu
kikanuni) lakini pia kutoa masuluhisho ya matatizo ya nchi yetu na
kusukuma kupitia Bunge mabadiliko chanya yanayotakiwa ili kuleta
mabadiliko nchini.
Ni
matumaini yangu kwamba Watanzania wanaoishi nje ya nchi, kokote walipo
watashiriki pamoja nasi katika vuguvugu (movement) hili la kuleta
mabadiliko katika Taifa letu. Hampaswi kukaa na kutazama, bali mnapaswa
kushiriki kikamilifu maana hii ni nchi yetu sote. Ni wajibu wa kila
mmoja wetu kuhakikisha nchi yetu inakuwa na demokrasia na ustawi wa watu
wake.
Hali ya Uchumi wa Nchi
Tumekuwa
moja ya nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi duniani. Katika
kipindi cha muongo mmoja uliopita uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa
wastani wa asilimia 6. Kazi hii ya ukuaji ukilinganisha na kiwango cha
ukuaji wa idadi ya watu (ambacho ni 2.8%) ingeweza kupunguza umasikini
kwa zaidi ya 50% katika kipindi hicho. Hata hivyo Umasikini Tanzania
umebakia ni mkubwa ambapo zaidi ya Watanzania 37 katika kila Watanzania
100 hawana uhakika wa mlo mmoja kwa siku. Idadi ya Watanzania masikini
wa kutupwa (wenye kipato cha chini ya tshs 500 kwa siku) imeongezeka
kutoka watu milioni 12 mwaka 2007 mpaka watu milioni 15 mwaka 2011.
Ukitaka kujua wingi huu ni wa kiwango gani, chukua idadi ya watu wa Nchi
ya Botwasana, Namibia, Swaziland na Lesotho haikaribii idadi ya
Watanzania wenye mashaka ya mlo mmoja kwa siku. Idadi ya watu wa
Denmark, Netherlands, Norway na Uholanzi kwa pamoja ndio sawa na idadi
ya Watanzania masikini. Kwa nini?
Ni kitendawili. Ni nadra kukuta uchumi unaokua kwa kasi kama wetu ukizalisha masikini zaidi. It’s a paradox of a fast growing economy and increasing poverty.
Kwa miaka kumi ambayo tumeiangalia (2000 – 2010) tumeshuhudia kwa
dhahiri kabisa kushindwa kwa sera za kuondoa umasikini zinazotekelezwa
na Serikali ya CCM.
Masikini
wa Tanzania wapo vijijini zaidi. Uchumi wa vijijini kwa kipindi cha
muongo mmoja umekua kwa wastani wa asilimia moja tu. Flat lining.
Kwa hiyo uchumi unaokua hivi sasa sio uchumi wa Watanzania bali ni
uchumi wa watu wachache kwenye sekta chache kama madini, mawasiliano na
ujenzi. Watanzania walio wengi walioko vijijini wanaendelea kuandamwa na
ufukara bila juhudi mahususi za kuwasaidia. Tumesema na tunarudia
kusema kwamba ni lazima kubadili mwelekeo wa mipango yetu na kujikita
kwenye maendeleo vijijini. Kama chama tunaendelea kusema jambo hili
ndani ya Bunge na pia kuwaelimisha wananchi kwenye mikutano yetu ya
hadhara.
Mfumuko
wa Bei umefikia kiwango cha juu sana cha 19% na hivyo hata mikopo
katika mabenki imekuwa ghali hadi kufikia riba ya 23% na zaidi. Mfumuko
wa bei unaongozwa na bei ya vyakula. Katika hali ya kawaida, kupanda kwa
bei za vyakula kungemnufaisha mkulima lakini hali sio hiyo Tanzania.
Mkulima bado anauza mazao yake kwa bei za vijijini ambazo ni ndogo na
zinaamuliwa na wachuuzi wa mijini. Lakini mkulima huyu anaponunua bidhaa
za matumizi yake kama sukari, mafuta ya taa, nguo nk ananunua kwa bei
za mijini ambazo zimeathiriwa vikali na mfumuko wa bei. Hivyo mfumuko wa
Bei unamuathiri zaidi mwananchi masikini kabisa. Serikali imekuwa
mlalamikaji kama wananchi wengine. Mfumuko wa Bei utapungua kwa kuongeza
uzalishaji wa chakula, kuimarisha miundombinu ya vijijini na kupunguza
gharama za Nishati kama hasa Umeme. CHADEMA inaendelea kuisukuma
Serikali kuchukua hatua ili kupunguza makali ya maisha kwa wananchi.
Hatua za muda mfupi zihusishe nafuu ya kodi kwenye bidhaa zinazotumiwa
na wananchi kwa wingi.
Hata
hivyo bado matumizi ya Serikali ni makubwa mno kwenye masuala ambayo
hayana uhusiano na kuendeleza watu. Bado bajeti ya posho mbalimbali,
safari za nje na hata matumizi makubwa ya magari ya serikali ni kubwa
mno kulinganisha na hali yetu ilivyo. Katika matumizi haya pia kuna
ufisadi mkubwa sana. CHADEMA inaendelea kuanisha masuala haya na kukemea
na kuchukua hatua pale inapobidi.
Uwezo
wetu wa kukusanya mapato ni changamoto kubwa. Mapato mengi yanapotea
kama misamaha ya kodi ambayo sasa imefikia tshs 1.3trn kwa mwaka. Mapato
mengine hayakusanywi kwa sababu ya ukwepaji kodi uliokithiri. Kodi
kwenye Sekta ya Madini imekuwa ni mjadala wa muda mrefu sana. Sheria ya
madini ya mwaka 1998 na Sheria za Fedha ya mwaka 1997 ziliweka mfumo wa
kinyonyaji kabisa ambao ulikuwa unafaidisha makampuni ya uchimbaji
madini kuliko Taifa. Sheria mpya ya madini ya mwaka 2010 ambayo
ilitokana na kazi kubwa tuliyofanya ndani ya Bunge pamoja na Mashirika
yasiyo ya kiserikali imeweka mfumo bora zaidi. Hata hivyo makampuni ya
Madini yaliweka mgomo kwenye sheria mpya kwa kukataa kuanzisha miradi
mipya na hata kukataa kuhamia kwenye sharia mpya. Sheria mpya inataka
Serikali kuwa na hisa kwenye kila mgodi, hisa za kampuni za madini
kuorodheshwa katika Soko la hisa la Dar es Salaam na kulipwa kwa mrahaba
mpya wa asilimia 4 kwa kanuni mpya ya kukokotoa mrahaba (from Netback
Value to Gross value) ambayo ingeongeza mapato ya Serikali maradufu. Kwa
miaka Serikali imekuwa inapoteza mapato kwa kutotekelezwa kwa sharia
mpya. Nimesikia kuanzia mwezi huu kampuni ya Barrick imeanza kulipa
mrahaba mpya. Tutataka maelezo ya Serikali kuhusu kampuni nyingine na
pia mrahaba wa miaka ya nyuma. Ni lazima Serikali ihakikishe nchi
inafaidika na rasilimali zake.
Tunaenda
kwenye Uchumi wa Gesi Asilia. Makampuni mawili makubwa duniani
yamegundua Gesi Asilia nchini kwa kiwango kikubwa sana. Hivi sasa
Tanzania ina Utajiri wa Gesi ulitothibitishwa wa 20TCF na makadirio
yanaonyesha kuwa tutafika 85TCF katika kipindi kifupi sana. Bado kuna
meneo yanaendelea kufanyiwa utafutaji kutokanana vitalu vilivyogawiwa.
Hata hivyo hatuna Sera na Sheria ya kusimamia vema sekta hii na hasa
yenye kuhakikisha Uwazi na Uwajibikaji. Hatuna pia Sheria ya kusimamia
mapato yanayotokana na Gesi Asilia (Petroleum Revenue Management Act).
Hatutaki kurudia makosa yaliyofanyika kwenye sekta ya Madini. Tunataka
Gesi Asilia itumike kwa maendeleo ya watu wetu.
Tumependekeza
kwamba Vitalu vipya vya kutafuta mafuta visitolewe kwa sasa
(moratorium) mpaka hapo Sera mpya, Sheria mpya na mfumo bora wa matumizi
ya Fedha zitakazotokana na Mafuta na Gesi ziwepo. Pia shughuli za
utafutaji katika vitalu vya sasa zitaongeza thamani ya vitalu vijavyo na
hivyo nchi kufaidika zaidi. Tumependekeza pia kwamba ni lazima kuweka
mfumo mzima wa uwazi na uwajibikaji katika sekta ili kujipanga vyema na
kuepuka yaliyowakuta wenzetu wenye utajiri kama huu ambao uligeuka
balaa. Tatu tumependekeza kusomesha Watanzania kwa ngazi zote. Mafundi
mchundo kupitia VETA na Mafundi wa kati kupitia Vyuo vya Ufundi. Muhimu
zaidi tunataka kijengwe Chuo Kikuu kikubwa Mtwara chenye Kampasi Lindi
ambacho kitakuwa ni kituo cha kufundisha sio watanzania tu bali Waafrika
wengine kuhusiana na masuala haya. Ujenzi wa Chuo Kikuu Mtwara unapaswa
kuanza mara moja bila kuchelewa.
Kutokana
na uzoefu tuliupata katika sekta ya Madini na kupitisha sharia mbaya
Bungeni, tunaona kwamba suala la Gesi tukabe kila mahala ili kuhakikisha
nchi inafaidika. Historia inatuonyesha kwamba Nchi nyingi za Kiafrika
zenye utajiri wa Gesi na Mafuta hazina demokrasia, zimegubikwa na uvundo
wa ufisadi na watu wake ni masikini. Tunataka kuonyesha Dunia kwamba
inawezekana kuwa nan chi ya Kiafrika yenye utajiri mkubwa wa Mafuta na
Gesi na ikawa ya kidemokrasia, isiyo na ufisadi na yenye watu wenye
ustawi. Sio kazi rahisi lakini tumedhamiria. CHADEMA haitakaa tu kuona
utajiri wan chi unatapanywa hovyo. Tumesema na kusimamia kwenye Madini,
tunatoa mwongozo kwenye Mafuta na Gesi.
Katiba
Ninajua
Watanzania mnaoishi nje mna shauku kubwa ya kujua ushiriki wenu na
hatma yenu kwenye Katiba mpya. Kwa muda mrefu mmekuwa mkishawishi haki
ya kupiga kura, haki ya kuwa na uraia zaidi ya mmoja (Dual Nationality)
na hata namna gani mnashiriki katika kujenga uchumi wa nchi.
Kwanza
nataka niwapongeze kwa kuchukua uamuzi mzito wa kuondoka nyumbani kuja
ughaibuni kutafuta maisha au maarifa au vinginevyo. Nawapongeza zaidi
kwa juhudi mnazofanya kusaidia familia zenu nyumbani, vijiji vyenu na
hata Taifa kwa ujumla. Takwimu zilizotangazwa na Benki Kuu ya Tanzania
zinaonyesha kwamba Watanzania mliopo nje ya Tanzania mlituma nyumbani
fedha (remittances) zaidi ya Dola za kimarekani 350 milioni mwaka 2011.
Hii ni sawa na asilimia 5 ya mapato yote ya Fedha za kigeni zilizoingia
Tanzania mwaka huo na ni zaidi ya Fedha za kigeni zilizoingizwa na Chai,
Kahawa, Pamba na Korosho kwa ujumla wake. Kwa hiyo ‘Diaspora’ ni sehemu
muhimu sana ya Uchumi wa Taifa ni muhimu Dola iwawekee mazingira mazuri
ya kuweza kufanikisha mambo yenu huku ili mshiriki vema maendeleo ya
nchi yetu.
CHADEMA
tunatambua umuhimu wenu hata kama msingekuwa mnatuma fedha nyumbani.
Ninyi ni Watanzania na ni jukumu la Dola ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuwalinda popote mlipo duniani. Mtakumbuka mwanzo mwa miaka ya
2000 kulikuwa kuna ‘petition’ ya kudai Uraia wan chi mbili kwa
Watanzania. Dkt. Willibrod Slaa alikuwa ni mmoja wa Wabunge waliokuwa
wanauliza maswali Bungeni kuhusu jambo hilo. Wengi tuliweka sahihi
katika ‘petition’ ile ambayo ilianzishwa na Watanzania wanaoishi nje.
CHADEMA inaunga mkono haki ya Watanzania kuwa na uraia wa nchi nyingine.
CHADEMA inataka suala hili lifikie mwisho kwenye mjadala wa Katiba.
Kuna watu wanasema sio uzalendo Mtanzania kuchukua uraia wa nchi
nyingine. Ninasema sio uzalendo pia kuacha raia wako wanateseka nchi
nyingine kwa sababu tu wamechukua uraia wa huko au wanashindwa kuchukua
uraia wa huko. Sheri zetu za Uraia ni gandamizi hasa kwa wanawake wa
Tanzania. Tumepoteza dada zetu wengi sana na watoto wao kwa sababu
wakiolewa na wageni watoto wao hawana haki ya kuwa raia. Wakinyanyaswa
na wageni na kutaka kurudi nyumbani wao na watoto wao wananyanyaswa pia
kwao. Haikubaliki na tutakabili suala hili kwa nguvu zetu zote. Tunataka
Watanzania walioko nje wapate kila aina ya msaada kutoka Dola yetu ili
wafanikiwe.
CHADEMA
inataka pia Watanzania waliopo nje waruhusiwe kupiga kura nyakati za
uchaguzi. Ni suala la ushamba tu kuendelea kujadili jambo hili la uwazi
kabisa. Kuna teknolojia za kisasa kabisa kuhakikisha watu wanapiga kura
kokote walipo. Mwaka 2004 Chama rafiki cha CHADEMA kutokan Msumbiji
RENAMO kiliniteua kuwa wakala wa kura katika kituo cha Ubalozi wa
Tanzania Msumbiji uliopo Dar es Salaam. Raia wa Msumbiji wanaoishi
Tanzania wanapiga kura nje, seuze Tanzania? CHADEMA inawahakikishia
kulisimamia jambo hili.
Katika
mkutano wa Bajeti ujao Bajeti Kivuli itazungumzia namna ya kuimarisha
uwekezaji wa Watanzania wanaoishi nje katika uchumi wa nchi. Siku zote
tunazungumzia mitaji kutoka nje kwa maana ya ‘Foreign Direct
Investments’ peke yake na kwa kweli tunasahau kwamba kuna ‘Diaspora
Direct Investments’. Tumetoa vivutio vingi sana kwa Wawekezaji kutoka
nje. CHADEMA inakwenda kupendekeza kuwepo kwa vivutio vya kikodi na
kirasimu kwa Watanzania wanaoishi nje wanaotaka kuwekeza nyumbani.
Ninawashawishi muangalie namna ya kujikusanya na kuwa na ‘Investments
Funds’ ili kununua ‘equties’ kwenye miradi mbalimbali. Uwekezaji
Tanzania unalipa sana (Return on Investments goes up to 25%) kwenye
baadhi ya maeneo. Huduma katika sekta zinazoinukia kama Mafuta na Gesi
ni eneo ambalo mnapaswa kuliangalia tusiachie wageni tu. Mnakumbuka
wakati wa mwanzo wa Sekta ya Madini hata huduma za kufua nilikuwa
zinatolewa na kampuni kutoka Australia! Mtwara hakuna vyumba vya kutosha
vya mahoteli na hata nyumba za kupanga, angalieni maeneo haya maana
Mtwara is booming. Sisi kama wanasiasa jukumu letu ni kuwawekea
mazingira mazuri. Ninyi mnapaswa kuzileta hizo Dola kidogo mpatazo
nyumbani na kuwekeza kwenye maeneo yatakayozalisha ajira na hivyo
kuondoa umasikini kwa ndugu zenu. Ninaamini mtachukua changamoto hii na
kuangalia namna ya kuitekeleza. Wenzetu kutoka Ethiopia na Kenya
wanafanya hivi.
Mjadala
wa Katiba pia na hatimaye Katiba mpya itaamua hatma ya Muungano wetu.
Muungano pekee katika Bara la Afrika ambao umedumu na umeonyesha nia ya
Mwafrika kukataa mipaka ya kikoloni. Kuna Watu wanaona Muungano huu
haina manufaa hivyo uvunjwe. Kuna watu wanaona ni bora kuurekebisha ili
uweze kufaidisha Jamhuri mbili zilizoungana. Mchakato wa Katiba mpya
kupitia Tume ya Katiba ambayo CHADEMA tumeshiriki, ni nafasi ya kuandaa
mustakabali wa Tanzania ijayo. Tanzania tunayoitaka kwa miaka mingine
hamsini, mia moja au hata alfu moja. Watanzania wawe huru kusema
wanataka Muungano au hawautaki, wanataka Muungano wa namna gani na
wanataka Tanzania ya namna gani.
Ni
Haki ya Watanzania wanaoishi nje kutoa maoni yao kuhusu Katiba. CHADEMA
inakusudia kwanza kukusanya maoni ya wanachama wake walioko nje kuhusu
Katiba lakini pia kuitaka Tume ya Jaji Warioba kuja huku kukutana na
Watanzania na kupata maoni yao. Ni Haki yenu kutoa maoni na ninawaomba
mtumie haki yenu vizuri. Mtupe uzoefu wa nchi nyingine ambazo mmeishi na
kuweza kuona ni vipi tutaimarisha Dola imara ya Kidemokrasia yenye
kuleta ustawi wa watu wake.
Msimamo
wa CHADEMA ni Muungano wa Serikali Tatu. Hata hivyo katika mchakato
tulio nao sasa wanachama wa CHADEMA wana uhuru wa kutoa mawazo mapya na
kuboresha sera hii ya CHADEMA kuhusu Muungano. Muwe huru kabisa kutoa
maoni yenu.
Haki na Wajibu
Watanzania
mnaoishi nje mna haki na lazima Dola ilinde haki hizo lakini pia kama
Watanzania mna wajibu kwa nchi yenu. Ni wajibu wenu kushiriki kikamilifu
katika kuimarisha demokrasia nchini. Sisi wenzenu tumejitoa muhanga
katika eneo hili. Tumejenga taasisi zinazoitwa vyama vya siasa kwa zaidi
ya miaka ishirini sasa. Hatuchoki lakini tunahitaji ushiriki wenu.
Jambo hili sio kwa wanachama wa CHADEMA peke yake bali pia hata
wanachama wa vyama vingine mnaoishi hapa Marekani.
Hutakuwa
mwanachama bora wa CCM kwa kufanya kazi ya kuwachoma Watanzania wenzako
ambao ni wana mageuzi kwa viongozi kila wanapokuja kwenye ziara nje ya
nchi. Utakuwa mwanachama mzuri wa chama chako iwapo utawaambia viongozi
ukweli wa mambo na namna bora ya kuongoza n chi yetu.
Hamuitendei
haki Tanzania kwa kusemana, kusingiziana, kutetana na hata kugombana.
Wakati mwingine unapoona mijadala ya watu kwenye mitandao ya kijamii
unasinyaa. Unajiuliza sasa kama hawa ndio wapo kwenye mwanga sisi tulio
kwenye giza inakuwaje?
Fanya
kazi. Furahia maisha. Lakini kumbuka kuna nchi yenye barabara za
mashimo, yenye giza muda mwingi wa mwaka kuliko mwanga, yenye umasikini,
yenye viongozi wasiwajibika na wala rushwa. Ni nchi yako. Usiseme hii
ni kazi ya kina Zitto, Slaa, Mbowe, Nassari, Leticia na Msigwa. Kila mtu
ana wajibu wa kufanya kuisogeza mbele nchi yetu. Timiza wajibu wako kwa
namna unavyoona inafaa.
Nkrumah once said ‘organise, don’t agonise’ narudia hivyo kwa Watanzania mliopo Marekani. Organise for your motherland.
Tanzania yenye usawa wa fursa
Nimalizie
kwa stori yangu. Nilizaliwa katika umasikini wa kutisha kama Watanzania
wengi wa vijijini. Nimekwenda shuleni bila viatu na wakati mwingi tumbo
likiwa tupu ama nimekunywa uji wa unga wa Yanga uliotiwa chumvi.
Darasani nilikuwa ninasoma na watoto wa watu wote wenye mamlaka pale
mjini Kigoma. Wote tulikuwa tunafundishwa na Mwalimu huyo huyo na
tunakaa darasa hilo hilo, tunapata elimu hiyo hiyo. Leo mimi ni msomi
mwenye shahada ya Uzamili na Mbunge nawakilisha watu wa kwetu. Wenzangu
wengi pia wanaendesha maisha yao na wengine wapo hapa Marekani
wakitafuta maisha.
Leo
mtoto wa masikini Tanzania hapati elimu anayopata mtoto wa mwenye
uwezo. Mtoto wa masikini hakutani na mtoto wa mwenye uwezo. Wanasoma
shule tofauti. Wanafundishwa na walimu tofauti. Hawachezi pamoja. Wote
wakimaliza kidato cha Sita, mtoto wa mwenye uwezo ana nafasi kubwa zaidi
ya kupata mkopo kwenda Chuo Kikuu kwa sababu amesoma shule bora zaidi
hivyo anapata daraja kubwa zaidi la kupewa mkopo na Bodi ya Mikopo.
Wakati
nasoma, kikwazo kilikuwa uwezo wako tu kichwani. Hivi sasa kikwazo ni
kipato pia. Tofauti ya kipato nchini ni kubwa lakini sisi wanasiasa
hatuioni. Wakati wenzetu wanajiandaa kufaidika na ‘demographic dividend’
kwani watoto wao wanapata elimu bora, sisi hata hatujiandai na
‘demographic Bomb’ litakaloletwa na kundi kubwa la vijana wasio na elimu
wala ujuzi.
Shiriki
kurejesha Tanzania yenye kutoa fursa kwa kila raia bila kujali hali
yake ya kipato. Shirika kurejesha Tanzania yenye Usawa kwenye fursa na
yenye demokrasia. Jiunge na CHADEMA tuendeleze mapambano.
Nawashukuru kwa kunisikiliza
Zitto Kabwe, Mb
Naibu Katibu Mkuu CHADEMA
0 comments:
Post a Comment