KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbroad
Slaa, amesema harakati za kuendesha mchakato mzima wa ‘Vua gamba, Vaa
gwanda’ ni lazima zikiguse pia Chama cha Wananchi (CUF) kwa vile
kimeungana na CCM na kushindwa kutetea masilahi ya wananchi hususan
wakazi wa mikoa ya Mtwara na Lindi.
Akihutubia
mkutano wa hadhara katika Kata ya Mkanaledi mkoani Mtwara jana, Dk.
Slaa alisema tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Chama
cha CUF kilipata uungwaji mkono kwa kiasi kikubwa na wakazi wa kusini
hivyo kushindwa kutetea masilahi yao na kuungana na CCM ni sawa na
kuwaambia wananchi wajitafutie ukombozi mwingine.
“CUF
tulikubaliana nao, kwakuwa wote ni wapinzani na wao wana nguvu huku na
maeneo ya pwani ni vema tukawaachia ili waendeleze jukumu la kuwakomboa
Watanzania,” alisema Dk. Slaa na kuongeza:
“Ndio
sababu hatujawahi kuweka mgombea urais katika uchaguzi wowote kwa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, lakini kitendo cha CUF kuungana na CCM
kimeonyesha dhahiri hawana nia ya kuwakomboa Watanzania,” alisema.
Dk.
Slaa alisema wakati wa wakazi wa Mtwara, Lindi na maeneo mengine
kuendelea kunung’unika umepita na kinachotakiwa ni kuchukua maamuzi
magumu kwa kuikataa CCM na kujiunga na CHADEMA.
Akizungumzia
rasilimali za mikoa ya kusini, Dk. Slaa alisema mikoa ya Lindi na
Mtwara inaongoza kwa kuzalisha zao la mihogo na korosho na kama mazao
hayo yangetumika vema yangesaidia kuleta maendeleo.
“Ninyi
mna rasilimali za kutosha sasa kama gesi, mihogo na bandari hizi
zikitumika ipasavyo hakuna kati yenu atakayelalamikia huduma mbovu za
serikali lakini hamna kinachofanyika,” alisema Dk. Slaa.
Alisema
serikali haikuwa na nia ya kweli ya kuwasaidia wananchi ndiyo maana
ikaamua kuuza kiwanda cha kubangulia korosho kwa Mama Anna Mkapa kwa
shilingi milioni 50 huku wananchi wakiendelea kutaabika.
0 comments:
Post a Comment